SHERIA ZA FUNGA NA ADABU ZAKE

Baada ya kumshukuru Allah Subhana Wataala na kumsalia Mjumbe wake Sayyidna Muhammad s.a.w. pamoja na sahaba zake na kila anayefuata njia yake

Umma wa Kiislamu:

Tambueni ya kwamba (taqwa) uchamungu una cheo kikubwa katika dini ya kiislamu , na wachamungu wana daraja za juu kwa mujibu wa maelezo ya qur-ani, kwa hivyo wachamungu ndiyo vipenzi vya Allah:

إن أولياؤه إلاّ المتّقون .

Hawakuwa walinzi wake isipokuwa wachamungu tu .

Na wachamungu ndiyo vipenzi vya Allah:

والله وليّ المتّقين .

Na Allah ni rafiki wa wale wamchao .

Na kwa hivyo watafuzu kukubwa mno siku ya kiama:

والآخرة عند ربّك للمتّقين .

Na akhera iliyo kwa mola ni ya wenye kumcha Allah .

Na ilivyokuwa funga ni njia imfikishayo mtu katika uchamungu , basi huwa ni wajibu kwa muislamu kuitekeleza vile ipasavyo , na ajitahidi kikomo cha uwezo wake katika kufuata adabu zake na kutochupa mipaka yake , ili funga yake imfikishe katika daraja za wachamungu na imuepushe na moto na kumtia katika pepo , anasema Allah Mtukufu:

فمن زحزح عن النار وأدخل الجنة فقد فاز ، وما الحياة الدنيا إلا متاع الغرور .

Na aliyewekwa mbali na moto na akaingizwa peponi , basi amefuzu . Na maisha ya dunia hii si kitu ila ni starehe idanganyayo .

Ndugu Waislamu:

Hakika funga inayofungwa na waislamu wengi siku hizi , sio hiyo funga inayotakiwa hasa kisheria , kwa sababu funga zao hazizidi zaidi ya kujizuwia na kula na kunywa na huupitisha mchana wao kwa uvivu na kutojishughulisha na kazi yoyote , mpaka linapokuchwa jua huanza kuvamia vyakula vya kila namna kisha hukesha usiku wake katika starehe na mchezo , basi mtu wa namna hii hutoka katika ramadhani kama alivyoingia , hakupata maghfira wala hakuufikia uchamungu .

Kwa hivyo ni vyema tutambue kuwa funga ambayo amewaamrisha Allah waja wake kuifunga , na ikawa ndiyo njia imfikishayo mtu katika uchamungu na kumuepusha na moto , ina adabu zake na mipaka yake na ina shuruti na ahkamu zake , kwa hivyo funga ni kujizuwiya na yale yote yenye kufunguza katika wakati wake maalumu , pamoja na kujuwa ulifanyalo na kutia nia . Na miongoni mwa sheria za funga ni kujizuwiya na kuingiza kitu chochote katika tundu ya mwili ifikishayo ndani ya tumbo , ikiwa kitu hicho ni chakula au si chakula , na inakatazwa kutoa kitu ndani ya tumbo kwa makusudi kama kujitapisha , na anatakiwa mtu anapokuwa ndani ya funga , ajizuwiye na maingiliano baina yake na mkewe au kujitowa manii kwa makusudi .

Na ikiwa kitaingiya kitu tumboni bila ya kukusudia , basi huwa hapana kitu kwa aliyefunga kwa mfano makohozi ikiwa hayakufika mdomoni bali yamepita kooni , ama yakifika mdomoni basi ni lazima ayateme na inakatazwa kukusanya mate kisha kuyameza na kwa aliyetapika bila ya  kukusudia huwa hapana neno isipokuwa asikimeze kile kilichobaki mdomoni , imekuja katika hadithi kutoka kwa Mtume s.a.w. amesema:

من ذرعه القيء فليس عليه قضاء ، ومن استقاء فليقض .

Aliyetapika bila ya kukusudia huwa hapana kitu , na kwa aliyejitapisha kwa makusudi basi alipe .

Na aliyefunga anatakiwa wakati wa kutia udhu asipeleke sana maji katika pua .

Na inampasa kwa aliyefunga kujiepusha na kila linaloamsha matamanio , kwa sababu kujitoa manii kwa makusudi kunaharibu funga , na kwa aliyepatwa na janaba mchana wa ramadhani akimbilie kuoga , na kwa aliyelala na mkewe anatakiwa kuoga kabla ya kupambazukiwa na alfajiri kama ilivyokuja katika hadithi sahihi isemayo :

من أصبح جنبا أصبح مفطرا .

Atakayepambazukiwa hali ya kuwa na janaba huwa amepambazukiwa akiwa hana funga .

Ndugu Waislamu:

Kwa hakika kuna jambo linamfunguza aliyefunga ambalo wengi wetu tumeghafilika nalo , na huharibu funga za watu kama alivyosema Mtume s.a.w. :

ربّ صائم حظّه من صيامه الجوع والعطش ، وربّ قائم حظّه من قيامه السّهر .

Huwenda kwa aliyefunga ikawa sehemu yake ni kukaa na njaa na kiu na huwenda kwa anayesimama kwa ajili ya kusali ikawa sehemu yake ni kukesha tu.

Kwa hivyo maasi na makosa hubatilisha funga anasema Mtume s.a.w.:

لا صوم إلا بالكف عن محارم الله .

Hapana funga ila kwa kujizuwiya na makatazo ya Allah .

Na amesema vilevile :

من لم يدع قول الزور والعمل به فليس لله حاجة أن يدع طعامه وشرابه .

Asiyewacha kusema uongo na vitendo vyake basi Allah hana haja ya mtu kuwacha chakula na kinywaji chake .

Na yametajwa baadhi ya madhambi yavunjayo funga kwa mfano :

الغيبة تفطّر الصائم وتنقض الوضوء .

Kusengenya kunamfunguza aliyefunga na kunaharibu udhu .

Na anatakiwa anayefunga ajiepushe na kulipa uovu aliotendewa imekuja katika hadithi :

فإذا كان يوم صوم أحدكم فلا يرفث ولا يصخب ، فإن سابّه أحد أو قاتله فليقل إنّي صائم .

Anapokuwa mmoja wenu katika funga asitukane wala asigombane , na akitukanwa au akitakiwa kupigana basi aseme mimi nimefunga .

Kwa hivyo hadithi hizi na nyenginezo ni dalili ya kwamba maasi yanaharibu funga na kupoteza ujira wake na humzuwia mtu kuufikia uchamungu .

Na funga ina wakati wake uliowekwa na sheria , huanza kwa kuchomoza alfajiri ya kweli na humalizika kwa kukuchwa jua , anasema Allah

وكلوا واشربوا حتّى يتبيّن لكم الخيط الأبيض من الخيط الأسود من الفجر ثمّ أتموا الصّيام إلى الّليل .

Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku . Kisha timizeni saumu mpaka usiku .

Na katika sunna za funga ya ramadhani ni kuchelewesha daku ili apate kuwa na nguvu wakati wa mchana , na ni sunna vilevile kuharakiza kufutari ikiwa wakati umeshafika ,anasema Mtume s.a.w. :

لا تزال أمّتي بخير ما عجّلت الإفطار وأخّرت السحور .

Bado ingali umma wangu watabaki katika kheri madhali wanafuturu mapema na wanachelewesha daku .

Na ni wajibu kuwa na yakini wakati wa kufutari kwamba wakati umeshaingia kwa sababu asili ni kubakia mchana na hairuhusuwi kula mpaka ithibiti kuingia kwa wakati wa usiku . Na Haifai kufanya israfu katika vyakula na vinywaji wakati wa kufutari , kwani Allah amekataza hayo katika kauli yake :

يا بني آدم خذوا زينتكم عند كلّ مسجد وكلوا واشربوا ولا تسرفوا إنّه لا يحبّ المسرفين .

Enyi wanaadamu! Chukueni mapambo yenu (vaeni nguo zenu)wakati wa kila sala , na kuleni na kunyweni vizuri . Lakini msipite kiasi tu , Hakika yeye Allah hawapendi wapitao kiasi .

Na Amesema Allah:

إنّ المبذّرين كانوا إخوان الشّياطين وكان الشّيطان لربّه كفورا .

Hakika watumiao kwa ubadhirifu ni ndugu wa mashetani . Na shetani ni mwenye kumkufuru Mola wake .

Kwa hivyo kuandaa kila aina ya vyakula na vinywaji katika ramadhani na baadae kutupwa chakula kilichobaki ni tabia inayokatazwa na sheria na hupoteza lile lengo hasa la funga .

Na inashurutizwa kuwepo na nia wakati wa kufunga imepokewa kutoka kwa Ibni Omar kutoka kwa ndugu yake hafsa kwamba Mtume s.a.w. amesema :

من لم يبيّت الصّيام من الّليل فلا صيام له .

Asiyetia nia ya funga tangu usiku basi huwa hana funga .

Basi mcheni Allah ndugu waislamu na jitahidini kuitekeleza ibada hii tukufu kwa adabu zake na sheria zake mtafaulu hapa duniani na kesho akhera .

والــســلام عـلـيـكـم ورحـمـة اللّه وبـركــاتــه