عذاب القبر
ADHABU YA KABURINI
بسم الله الرحمن الرحيم
|
Enyi waja wa Mwenyezi Mungu! Mcheni Mwenyezi Mungu na mumuogope, mutii amri zake msimuasi, mumshukuru msimkufuru, mumkumbuke msimsahau. Na mjue kwamba mwanaadamu ameumbwa aishi umri wake, kisha marejeo yake yawe kwenye shimo jembamba akapumzike humo au akaadhibiwe hadi siku ya malipo. Mwanaadamu akiishi maisha haya katika hali ya kutii amri za Mola wake, akitaraji rehma zake na kuogopa adhabu yake, Mwenyezi Mungu humsalimisha na yale anayoogopa na kumtimizia yale anayotaraji, na kwa hiyo roho yake inapotoka huambiwa: { يَا أَيَّتُهَا النَّفْسُ المُطْمَئِنَّةُ ، ارْجِعِي إِلَى رَبِّكِ رَاضِيَةً مَرْضِيَّةً ، فَادْخُلِي فِي عِبَادِي ، وَادْخُلِي جَنَّتِي } [1] (Ewe nafsi yenye kutua! Rejea kwa Mola wako hali ya kuwa umeridhia na umeridhiwa. Haya ingia katika waja wangu, uingie katika Pepo yangu) Na huyo hupumzika na huzuni za dunia na shida zake. Ama akiishi katika hali ya kumuasi Mwenyezi Mungu s.w. na kupinga amri zake basi ni maangamivu na shida iliyoje itakayompata! Huyo mpe habari ya kauli ya Mwenyezi Mungu s.w.: { وَلَوْ تَرَى إِذِ الظَّالِمُونَ فِي غَمَرَاتِ المَوْتِ وَالمَلاَئِكَةُ بَاسِطُو أَيْدِيهِمْ أَخْرِجُوا أَنْفُسَكُمُ اليَوْمَ تُجْزَونَ عَذَابَ الهُوْنِ بِمَا كُنْتُمْ تَقُولُونَ عَلَى اللهِ غَيْرَ الحَقِّ وَكُنْتُمْ عَنْ آيَاتِهِ تَسْتَكْبِرُونَ } [2] ((Na kama ungewaona madhalimu wanapokuwa katika mahangaiko ya mauti, na malaika wamewanyoshea mikono yao (wakiwambia): "Zitoeni roho zenu! Leo mtalipwa adhabu idhalilishayo kwa vile mlivyokuwa mkisema juu ya Mwenyezi Mungu yasiyo kweli na vile mlivyokuwa mkizifanyia kiburi aya zake) Hivyo mtu dhalimu anapofikwa na mauti na roho ikafika kwenye koo huwa ameshatoka katika kipindi cha kufanya kazi na ameshaingia katika kipindi cha malipo; kwani anayekufa kiama chake huwadia na huyaona kwa macho yake yale yote aliyokuwa akikaidi na kubisha. Enyi waja wa Mwenyezi Mungu! Hakika adhabu ya kaburini ni kweli na hakika watu watapewa mtihani makaburini mwao, kisha kaburi huwa ama bustani kati ya mabustani ya Peponi kwa kila muislamu mcha Mungu, au shimo kati ya mashimo ya Motoni kwa kila kafiri na muovu. Na hayo ndio maisha ya barzakh, ambayo kipindi chake ni baina ya mtu kutolewa roho duniani hadi kurudishiwa tena roho wakati litakapopulizwa baragumu la kuhuishwa watu na kutolewa makaburini. Kati ya dalili za kuwepo adhabu ya kaburini ni kauli ya Mwenyezi Mungu s.w. kuhusu Firauni na watu wake: { النَّارُ يُعْرَضُونَ عَلَيْهَا غُدُوًّا وَعَشِيًّا } [3] (Moto wanachomewa asubuhi na jioni) Yaani baada ya wao kuangamizwa kwa kuzamishwa roho zao zinachomwa moto kila siku mara mbili: asubuhi na jioni mpaka siku ya kiyama. Moto unaokusudiwa katika aya hii ni moto wa kaburini na sio moto wa Jahannamu; kwasababu Mwenyezi Mungu s.w. anasema mwishoni mwa aya hiyo: { وَيَوْمَ تَقُومُ السَّاعَةُ أَدْخِلُوا آلَ فِرْعَوْنَ أَشَدَّ العَذَابِ } 3 ((Na siku kitakaposimama kiyama (kutasemwa): "Waingizeni watu wa Firauni katika adhabu kali zaidi")) Vile vile kauli ya Mwenyezi Mungu s.w. kuhusu wanafiki wa zama za Mtume s.a.w. waliokuwapo katika mji wa Madina na vitongoji vyake: { سَنُعَذِّبُهُمْ مَرَّتَيْنِ ثُمَّ يُرَدُّونَ إِلَى عَذَابٍ عَظِيمٍ } [4] (Tutawaadhibu mara mbili, kisha watarudishwa kwenye adhabu kubwa) Katika aya hii Mwenyezi Mungu s.w. ametaja kwamba wanafiki hawa wataadhibiwa mara mbili kisha watarudishwa kwenye adhabu kubwa. Hivyo adhabu ya mara ya mwanzo ni ya duniani, kwa kuwafichua na kuwadhalilisha, au kwa kuwaletea msiba, au kwa kuwatilisha adabu maalumu alizozipanga kwa makosa maalumu. Adhabu ya mara ya pili ni ya kaburi, na adhabu kubwa ambayo watarudishiwa ndio adhabu ya Moto baada kufufuliwa siku ya kiyama. Vile vile Mwenyezi Mungu s.w. ameyaelezea maisha ya starehe katika kipindi cha barzakhi kwa wale waliokufa mashahidi akasema: { وَلاَ تَحْسَبَنَّ الَّذِينَ قُتِلُوا فِي سَبِيلِ اللهِ أَمْوَاتًا بَلْ أَحْيَاءٌ عِنْدَ رَبِّهِمْ يُرْزَقُونَ ، فَرِحِينَ بِمَا آتَاهُمُ اللهُ مِنْ فَضْلِهِ وَيَسْتَبْشِرُونَ بِالَّذِينَ لَمْ يَلْحَقُوا بِهِمْ مِنْ خَلْفِهِمْ أَلاَّ خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلاَ هُمْ يَحْزَنُونَ } [5] ((Na usidhani kamwe kuwa wale waliouawa katika njia ya Mwenyezi Mungu ni wafu; bali wahai, wapo kwa Mola wao wanaruzukiwa. Wanafurahia aliyowapa Mola wao katika fadhila zake, na wanawafurahia wale ambao bado hawajaungana nao, walio nyuma yao (duniani), kwamba hakutakuwa na khofu juu yao wala hawatahuzunika)) Na kama Mwenyezi Mungu alivyowaneemesha hawa waliofuzu kwa maisha ya starehe katika kipindi cha barzakhi, basi Yeye pia ni muweza wa kuwafanya wale waliokosa waishi maisha ya adhabu makaburini mpaka kiyama kitakaposimama. Na katika yaliyokuja kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu s.a.w. kuhusu adhabu ya kaburini ni kauli yake s.a.w.: (Hakika mmoja wenu anapokufa huoneshwa makaazi yake asubuhi na jioni; kama ni katika watu wa Peponi basi ni katika watu wa Peponi, na kama ni katika watu wa Motoni basi ni katika watu wa Motoni, na huambiwa haya ndio makaazi yako atakapokufufua Mwenyezi Mungu siku ya kiyama). Vile vile Mtume s.a.w. amesema: [ لَوْلاَ أَنْ لاَ تَدَافَنُوا لَدَعَوْتُ اللهَ أَنْ يُسْمِعَكُمْ عَذَابَ القَبْرِ ] (Kama si kuwa hamtazikana, ningalimuomba Mwenyezi Mungu akusikizisheni adhabu ya kaburi) Na kuhusu mtihani wa kaburini Mtume s.a.w. anasema: (Hakika mja anapowekwa kaburini mwake, na wenziwe wakamwacha na kuondoka hali ya kuwa anasikia sauti ya viatu vyao wanapoondoka, malaika wawili humjia wakamkalisha na kumwambia: "Nini ulikuwa ukisema kuhusu mtu huyu?" - yaani Muhammad s.a.w. Basi aliye muumini husema: "Nashuhudia kuwa yeye ni mja wa Mwenyezi Mungu na mtume wake". Na hapo huambiwa: "Tazama mahala pako pa Motoni Mwenyezi Mungu amekupa badala yake mahala pingine Peponi", na huoneshwa mwahala mote muwili. Ama mnafiki na kafiri huambiwa: "Nini ulikuwa ukisema kuhusu mtu huyu?", na husema: "Sijui. Nilikuwa nikisema wasemavyo watu". Na hapo huambiwa: "Usijue wala usifuate!". Kisha hupigwa kwa nyundo ya chuma pigo moja la utosi apige ukelele atakaousikia kila aliye karibu nae isipokuwa wanaadamu na majini) Mwenyezi Mungu s.w. ameeleza kwamba Yeye huwathibitisha waumini katika mtihani wa kaburini kwa kauli thabiti na huwaacha kupotea madhalimu, aliposema s.w.: { يُثَبِّتُ اللهُ الَّذِينَ آمَنُوا بِالقَوْلِ الثَّابِتِ فِي الحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الآخِرَةِ وَيُضِلَّ اللهُ الظَّالِمِينَ وَيَفْعَلُ اللهُ مَا يَشَاءُ } [6] (Mwenyezi Mungu huwathibitisha wale walioamini kwa kauli thabiti katika maisha ya dunia na katika Akhera. Na Mwenyezi Mungu huwaacha kupotea madhalimu. Na Mwenyezi Mungu hufanya atakavyo) Mwenye kutaka athibitishwe na Mwenyezi Mungu s.w. kwa kauli thabiti atakayowajibia malaika wawili kaburini na kuepuka adhabu, hana budi kumuabudu Mwenyezi Mungu kwa kumtakasia nia katika ibada, na kuepuka makosa na mambo ya shari, na kushika utiifu na mambo ya kheri. Kwani mwerevu ni yule anayeimiliki nafsi yake akatenda yatakayomfaa baada kufa; na mjinga ni yule anayeiachia nafsi yake ipendavyo kisha akawa na matumaini mengi kwa Mwenyezi Mungu. Miongoni mwa makosa yanayowajibisha adhabu ya kaburi ni kufitinisha watu na kutojitakasa na mkojo. Imepokewa kuwa Mtume s.a.w. alipita kwenye makaburi mawili akasema: [ إِنَّهُمَا لَيُعَذَّبَانِ وَمَا يُعَذَّبَانِ فِي كَبِيرٍ ، أَمَّا أَحَدُهُمَا فَكَانَ لاَ يَسْتَبْرِئُ مِنَ البَوْلِ وَأَمَّا الآخَرُ فَكَانَ يَمْشِي بَيْنَ النَّاسِ بِالنَّمِيمَةِ ] (Hakika hawa wawili wanaadhibiwa, na hawaadhibiwi kwa jambo kubwa. Kwani mmoja wao alikuwa hajitakasi na mkojo, na mwengine alikuwa akifitinisha watu) Katika hadithi nyengine, Mtume s.a.w. anasema: [ اِسْتَنْزِهُوا مِنَ البَوْلِ فَإِنَّ عَامَّةَ عَذَابِ القَبْرِ مِنْهُ ] (Jitakaseni na mkojo; kwani adhabu ya kaburi aghlabu husababishwa na mkojo) Kutokana na hadithi hizo inabainika hatari ya mtu kufanya haja wima kisha asijinadhifishe ipasavyo. Mtume s.a.w. alikuwa mara nyingi anaomba kinga ya adhabu ya kaburi. Bibi Aisha r.anha amesimlia kuwa bibi mmoja wa kiyahudi alikuja nyumbani kwake akataja adhabu ya kaburi, na Mtume s.a.w. akasema: "Ndio, adhabu ya kaburi ni kweli". Amesema Bibi Aisha r.anha: "Na sikumuona Mtume wa Mwenyezi Mungu s.a.w. baada hapo akisali sala yoyote ila huomba kinga ya adhabu ya kaburi" Na imekuja amri katika Sunna kwa mwenye kusali aombe kinga ya mambo mane kabla kutoa salamu baada ya tashahudi ya mwisho; mojawapo ni adhabu ya kaburi. Katika hadithi Mtume s.a.w. amesema: [ إِذَا فَرَغَ أَحَدُكُمْ مِنَ التَّشَهُّدِ الأَخِيرِ فَلْيَتَعَوَّذْ مِنْ أَرْبَعٍ : مِنْ عَذَابِ جَهَنَّمَ ، وَمِنْ عَذَابِ القَبْرِ ، وَمِنْ فِتْنَةِ المَحْيَا وَالمَمَاتِ ، وَمِنْ شَرِّ المَسِيحِ الدَّجَّالِ ] (Atakapomaliza mmoja wenu tashahudi ya mwisho basi naaombe kinga ya mambo mane: ya adhabu ya Jahannamu, na ya adhabu ya kaburi, na ya mtihani wa uhai na mauti, na ya shari ya Masihi muongo) Mcheni Mwenyezi Mungu enyi waja wa Mwenyezi Mungu, na muliandalie kaburi amali njema itakayokuokoeni na adhabu ya kaburi na vitisho vyake. Kwani kaburi ni kizingiti cha mwanzo cha kuingilia Akhera; mtu akinusurika nacho, yafuatayo huwa mepesi zaidi; na asiponusurika, yafuatayo huwa magumu zaidi. Na mja hatajinusuru na adhabu ya Mwenyezi Mungu ila kwa kutekeleza amri zake na kuacha makatazo yake na kutanguliza amali njema. Imekuja katika hadithi ya Mtume s.a.w.: [ يَتْبَعُ المَيِّتَ ثَلاَثَةٌ : أَهْلُهُ وَمَالُهُ وَعَمَلُهُ فَيَرْجِعُ اثْنَانِ وَيَبْقَى وَاحِدٌ ؛ يَرْجِعُ أَهْلُهُ وَمَالُهُ وَيَبْقَى عَمَلُهُ ] (Vitu vitatu humfuata maiti: Watu wake na mali yake na amali yake, kisha viwili hurejea na kimoja hubaki. Hurejea watu wake na mali yake, na hubaki amali yake) [1]- الفجر / 27-30 [2]- الأنعام / 93 [3]- غافر ( المؤمن ) / 46 [4]- التوبة / 101 [5]- آل عمران / 169-170 [6]- إبراهيم / 27
|