MAMBO SITA YANAYOMWINGIZA
MTU PEPONI.
Mtume S.A.W. ametumwa kwa binadamu na Majini ili awangoze katika njia ya
haki itakayowatoa katika giza na kuwapeleka kwenye mwangaza wenye nuru
kisha kufuzu na kuingia katika Pepo ya Mwenyezi Mungu S.W.T. ambayo upana
wake ni sawa na mbingu na ardhi. Kwa hivyo Mtume S.A.W. ni Mtume wa umma
huu uliosifiwa na Mola Mtukufu na pia ni Mwalimu wetu anayetuongoza katika
mambo yote yanayohusu dini yetu ya Kiislamu. Lakini Mwislamu lazima
afahamu kwamba amekalifishwa kutenda mambo mengi mema tuliyofunzwa na
Mtume wetu ambaye hasemi neno lolote lile isipokuwa ni wahyi utokao kwa
Mola wa walimwengu wote na ni maslaha kwa umma. Katika mambo hayo mema
tumeahidiwa kwamba atakaetekeleza mambo sita basi bila shaka ataingia
Peponi. Ingawa mambo hayo sita ni mepesi kuyasema kwa ulimi wakati mtu
anaposoma kitabuni lakini kusema kweli ni magumu kuyatekeleza hasa kwa
wakati huu tulionao. Kwani baadhi ya watu hivi sasa wanachukulia kwamba
kusema uwongo kutamsaidia mtu kufanikisha lengo lake alilokusudia kama
vile kupandishwa cheo chake kazini au kufitinisha watu au kuwapokonya watu
mali yao. Na mara nyingi mtu anapoahidi mwishowe hushindwa kutekeleza hiyo
ahadi.
Ukweli ulivyo hayo yote binadamu anayokimbilia kuyatenda kinyume na
maamrisho ni kazi ya Shetani anayefanya bidii hiyo na kupandisha bendera
yake katika kila kona ya ulimwengu huu kwa kuwapotosha watu kutenda
yaliyoharamishwa kwa kuwapambia waja wa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwamba
wasiwe na wasiwasi wanayo fursa na umri mrefu wa kutubu, au hakuna lolote
huko Akhera uhai ni wa hapa tu duniani mtu akifa ndio mwisho wa uhai wake.
Siku hizi maasi mengi yameenea duniani kwa sababu watu wameacha dini yao
na mila yao na kufuata mitindo ya makafiri kwa kudhani kwamba wao ndio
watu walioendelea mbele kwa mavazi, maisha na mengi mengineo. Na ukweli
huu unaonekana wazi na kila mmoja wetu, kwani siku hizi majina ya vitu
vilivyoharamishwa yamegeuzwa kwa majina ya kupendeza kama vile: Zina
imeitwa mahaba, ulevi ni kiburudisha-moyo, sigara kiondosha-mawazo na
miziki ni utamaduni wa jadi. Na utaona watu waliowaiga hao makafiri hadi
wamefikia wanaume kuvaa hereni, kusuka nywele na kurefusha nywele zao kama
walivyo wanawake. Na haya yanawasababishia kusahau mipaka ya Mwenyezi
Mungu S.W.T. na kujipa moyo ati ulimwengu wa sasa umebadilika na kuendelea
mbele si kama ule wa zama za kale. Kwa hivyo mtu anakhiyari ya kufanya
lolote lile analoona linampendeza. Jamani! Hebu tuzinduke na kasumba hii
ya kuiga vitendo vya makafiri wanao upiga vita Uislamu na badala yake
tuige Sunna na adabu za Mtume wetu alizofunzwa na Mola Mtukufu Mtume
S.A.W. kasema:
"تكفلوا علي بست أتكفل لكم بالجنة. "قالوا: وما هي ؟ قال: "إذا حدث أحدكم فلا
يكذب ، وإذا وعد فلا يخلف ، وإذا إئتمن فلا يخون ، وغضوا أبصاركم ، وكفوا
أيديكم ، واحفظوا فروجكم".
Maana yake, “Nidhaminieni mambo sita nitakudhaminieni Pepo. Wakasema “Hayo
ni yapi?” Akasema “Akizungumza mmoja wenu asiseme uwongo, na akiahidi
asivunje miadi, na akiaminiwa asikhini, na inamisheni macho yenu (msitizame
yaliyokatazwa), na zuieni mikono yenu (msiendee mambo ya haramu) na
zihifadhini tupu zenu (msizini).”