HATARI YA KUMSHABIHISHA ALLAH

 

Shukurani zote ni kwa Allah aliyeumba kila kitu, asiyekua na mwanzo wa kuwepo kwake, na kila kitu ni kiumbe chake, hajafanana na kitu wala hakuna kitu kilichofanana na yeye, na Rehma na Amani ziwe kwa Mtume wetu Muhammad (s.a.w) aliyetumwa akiwa Rehma kwa Walimwengu wote, pamoja na Aali wake na Swahaba wake na kila anayefuata uongofu wake mpaka siku ya Malipo (Amin).

Kumshabihisha Allah mtukufu, ni kumfananisha yeye na mwengine asiyekua yeye, au mwengine kumfananisha na Allah.

Kumshabihisha Allah kunapatikana iwapo mtu ataitakidi kua Allah anasifika kwa sifa za Viumbe wake, kama vile kuwa yeye ana Umbo, au Mkono au Mguu au Mdomo au Pua, au kuwepo katika sehemu Fulani ikiwa ni Mbinguni au popote pale kama kukaa juu ya Kiti, au kuitakidi kua Allah anaondoka kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyengine, au kuitakidi kua Allah ataonekana kwa Macho, na mengineo mfano wa hayo.

Haya yote yamo katika hukumu ya Kumshabihisha Allah.

HATARI YA KUMSHABIHISHA ALLAH MTUKUFU

Hakika kumshabihisha Allah mtukufu ni hatari kubwa sana, na hatari hii inapatikana katika kuitakidi mambo yaliyoko nje na uhakika wa Allah, kwa hivyo kunapelekea katika upotevu, na mwisho wake ni kuporomosha utukufu wa Allah, na kuondosha Heshima yake, na kuitakidi nje ya ukweli ulivyo.

Na kumshabihisha Allah mtukufu ni mtihani walioupata wengi katika Umma zilizopita, hata unaposoma yale yaliyorithiwa katika maandiko yao utayaona haya kwa uwazi kabisa, zilifanya hayo kalamu za Waandishi, na Fikra za watu kwa kufuata mapendwa Moyo yao na kuitika wasiwasi wa Kishetani, hata ikapelekea kuitakidi kua Mungu yuko kama sisi katika Sura, Mfano na Namna, na kupelekea kuchonga Masanamu ili iwe ni njia ya kumuabudia Allah aliyeumba.

Na sio ajabu kuona Msiba wa kumshabihisha Allah kuwemo katika Umma huu vile vile katika baadhi ya maandiko, na pengine hata kuyasikia hayo katika baadhi ya Mihadhara ya Mashekhe, kwa hivyo tunapoyakuta tuwe macho tusije tukaingia katika Kosa hilo kubwa.

Na hatari ya Kumshabihisha Allah tunaweza kuileza katika haya yafuatayo:

1.     Kuondosha Upweke([1]) wa Allah.

Hili litapatikana ima kwa kuliitakidi kwa kujua au bila ya kujua, kwa sababu unapompa Allah sifa ya kumshabihisha tayari umeshaingia katika mlango wa kuitakidi kua Allah hakuumba vitu vyote, kwa sababu haiwezekani kuwepo bila ya kupatikana yale yaliyolazimika kupatikana katika kuwepo sifa ya kumshabihisha, kwa sababu sifa yoyote ya Kiumbe ina mambo yanayolazimika kuwepo ili ipatikane Sifa hiyo, kwa mfano Sehemu katika kupatikana Mkono au Mguu, kwa sababu vitu hivyo haviwezi kupatikana mpaka ipatikane Sehemu ambayo ni ulazima wa kupatikana kwake, Sasa unapoitakidi sifa ya kumshabihisha Allah tayari umeshavunja Upweke wake, na kumfanya Allah kua ni mwenye uwezo katika Baadhi ya Vitu tu, na kua yeye ameumba Baadhi ya Vitu tu, Ama vyengine kama Sehemu itakua sio Kiumbe kwa sababu vilikua pamoja na yeye kwani Kuumba ni Kitendo na Kitendo kinapatikana Baada ya Kuwepo Mtendeji. Allah atueke mbali na sifa potofu za kumshabihisha.

1: Upweke ni kua Allah yuko peke yake bila ya kushirikiana na chengine chochote katika kuepo kwake.

2.    Kuondosha sifa ya Ukwasi([2]).

Allah hahitaji kitu, na sifa za viumbe ni zenye kuhitaji, kwa sababu zinahitaji Sehemu, wakati, ..; na vile vile mwenye sifa hizo anakua yumo katika kuzihitaji, kwa hivyo unapoitakidi sifa ya Kumshabihisha Allah mtukufu tayari umeshaingia katika Mlango huu wa kuitakidi kua Allah anahitaji, hakika Allah ametakasika na kuhitaji.

2: Mkwasi ni kujitosheleza  bila ya kutegemea chochote.

3.   Kuitakidi Mabadiliko ya Allah.

Kwa kawaida Muislamu anaamini kua Allah ameumba kila kitu, na kua yeye ndiye wa Mwanzo, na kila kitu kisichokua yeye ni kiumbe, kwa sababu yeye ameumba kila kitu, na katika alivyoviumba ni vile vinavyolazimika kuwepo katika kuviumba viumbe vyake, kama vile Sehemu, sasa unapoingia katika mtego wa Kuitakidi sifa za kumshabihisha Allah, unajikuta tayari unamfanya Allah katika Fikra zako kua ni kama kiumbe yumo katika yale waliyomo viumbe, kwa hivyo ameshakua na sifa za kukubaliana na yale yanayokubaliana na viumbe, kwa hivyo amebadilika kutoka katika Hali ya kwanza kabla hajaumba na kuingia katika Hali ya pili katika kuumba na Baada ya kuumba, na hayo -sio kuongezeka Sifa za Vitendo lakini- ni mabadiliko ya Dhati yake, na kubadilika ni sifa iliyopatikana baada ya kukosekana, kwa hivyo Hali ya pili ilikua Haipo, kutokana na Hayo itakua Allah ana mwanzo kama sisi viumbe, na kuitakidi hivi ni Mizizi ya Ukafiri, Allah atuepushe nayo.

4.    Kujenga Sura ya Muumba katika Fikra ya mwenye kuitakidi.

Kwa hakika unapoitakidi Sifa ya kumshabihisha Allah tayari unajenga Sura katika Fikra yako, na kujenga Sura hiyo katika Kichwa ni Hatari kubwa sana, kwani tayari umeshampa Umbile na umeshamfanya kua ni mwenye kuhitaji, na kumpa kila sifa ambayo itamjaalia -katika fikra Zako- kua sawa sawa na Kiumbe, kwa hivyo kunapelekea kuabudu Sura, jambo ambalo halina tofauti na kuabudu Sanamu. Allah atuepushe na Fkra za Kishetani (Amin).

5.    Migongano na Waislamu.

Muislamu anapobeba Itikadi potofu ya Kumashabihisha Allah, anakua tayari ni kama jeshi lenye kubeba silaha ya kuwahujumu Waislamu, kwa sababu tayari ametofautiana nao katika Msingi Mkuu wa Uislamu, nao ni Kumuamini Allah katika ukamilifu wa Dhati yake na kua yeye hajafanana na chochote kile katika Viumbe vyake Kidhati, wala hakuna kiumbe kilichofanana na yeye, lakini mwenye kuchukua Itikadi hii sahihi -katika mtazamo wa mwenye kumshabihisha Allah- anakua Bado hajamjua Allah, kutokana na hapo anaanza kumshambulia kua yeye ni mwenye kuzipinga Sifa za Allah, na kua yeye Haabudu kitu, na kua yeye sio Muislamu, kwani bado hajamkubali Allah kwa kumjua katika Sifa zake, na hapo anakusudia zile Sifa za Kumshabihisha: Macho, Mikono, Miguu, Kuwepo katika sehemu, Kukaa katika Kiti, Kuteremka kwa kuondoka Katika sehemu Moja na kwenda katika Sehemu nyengine, kuonekana, n.k. Na mara nyengine  utawaona watu wenye itikadi hizi Wanawahukumu wale waliokhitalifiana nao kua sio Waislamu, kwa hivyo hata kusali nyuma Yao Haifai. Allah atueke Mbali na kila Fitna na kila Baya (Amin).

Ndugu yangu Muislamu jihadhari usije ukawa ni Askari wa Shetani katika kuchukua Itikadi ya Kumshabihisha Allah Mtukufu, na ukawa ni Sababu ya kuwatia Waislamu katika Hukumu ya Ushirikina, na ujue kua haya tumeyaandika kama ni njia ya kuchuka Hadhari kabla ya Kuja Athari, kwa sababu "Kinga ni Bora kuliko Tiba" kama walivyosema.

Tunamuomba Allah atueke mbali na fikra za Kumshabihisha na atueke Mbali na Fitna hiyo, na atujaalie tuwe ni kitu kimoja (Amin).

Asante sana.

Ndugu yenu: Hafidh. H. Seif  Sawafiy

Imam wa Msikiti  wa Bujumbura (Burundi)

Copyright ©2004  Uislam.net