(SIKU ZA TASHRIQ)

 

HUKUMU ZA SIKU YA 11, 12, NA 13 DHUL-HIJA

  -Kulala Mina siku za tashriq ni sunna iliyowajibishwa; asiyelala huko itamlazimu kuchinja.

  -Kulala kuliko lazima ni usiku wa kuamkia tarehe 11 na 12 kwa wenye haraka. Ama wasio na haraka ni usiku wa wa kuamkia tarehe 11, 12 na 13.

  -Inasuniwa kukithirisha takbir katika siku hizi katika kila hali.

  -Mwenye kuhiji atazipiga jamra tatu kila siku katika siku za tashriq kwa vijiwe ishirini na moja kila jamra vijiwe saba.

  -Ataanza kulipiga jamra dogo, kisha la kati, kisha jamra kuu.

  -Kupiga jamra siku hizi huwa baada ya kupindukia jua (adhuhuri) mpaka kutua jua, ikiwepo nafasi.

  -Ataomba dua baada ya kupiga jamra dogo na la kati, na haombi dua baada ya jamra kuu kutokana na alivyofanya Mtume - rehema za Allah na amani zimshukie.

  -Atazipiga tena jamra tatu kwa mpanglio huu katika siku mbili zilizobaki kwa asiye na haraka, na katika siku ya pili kwa mwenye haraka.

  - Mwenye kutaka kuharakiza kuondoka Mina itamlazimu atoke kabla kuzama jua; akichelewa atabaki mpaka siku inayofuata.

TAWAFU YA KUAGA:

 _ Mwenye kuhiji akimaliza kuzipiga jamra akataka kusafiri anapaswa aje kwenye Nyumba Takatifu atufu tawafu ya kuaga mizunguko saba.

 _ Tawafu ya kuaga ni sunna iliyowajibishwa; mwenye kuiacha itamwajibikia kuchinja, isipokuwa mwenye hedhi na mwenye nifasi inawajuzia kuiacha.

 _ Hapana ubaya katika kumbeba mgonjwa katika tawafu.

MAZINGATIO:

Atakayetufu tawafu ya kuaga na hakutimiza mizunguko saba inamlazimu kurudia tena tawafu yake. Asipoirudia mpaka akatoka Maka itamwajibikia kuchinja.

Akitaka mwenye kuhiji kupumzika katika kutufu kutokana na msongamano mkubwa au machofu hapana kitu juu yake, na itampasa aendelee alipofika katika tawafu yake ikiwa hajatengua udhu wake; ukitenguka atatufu tena upya baada ya kutawadha.

Hapana ubaya kwa aliyekwisha kutufu tawafu ya kuaga iwapo atakula au kunywa bila kununua; analozuiliwa ni kuuza na kununua.

Inajuzu kwa aliyekwisha kuiaga Nyumba Takatifu kusali hapo hata nafla (sunna), vilevile kuwasiliana kwa simu na kununua anachokihitaji katika safari ikiwa ni petroli au kinginecho ikimbidi. Hivyo mwenye kununua viatu asivyo budi navyo hapana kosa juu yake.

Inajuzu kuiaga Nyumba Takatifu kabla sala ya Ijumaa hata kama ataondoka baada ya sala ya Ijumaa.

Copyright ©2005  uislamu.net